WATUMISHI WA SERIKALI WASHAURIWA KUBADILI MTINDO WA MAISHA KULINDA AFYA ZAO
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka ametoa wito kwa watumishi wa umma kubadili mtindo wa maisha ikiwa ni pamoja na kujihusisha na michezo mbali mbali ili kulinda afya zao na hivyo kutoa mchango wao kikamilifu katika kuwahudumia wananchi.
Ametoa wito huo jijini Dodoma katika bonanza la Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kupitia hotuba iliyowasilishwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Ikulu, Bw. Majura Mahendeka.
Bonanza hilo ambalo limehusisha matembezi mepesi (jogging) kwa viongozi na watumishi wa serikali kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbali mbali za serikali kutoka katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limefanyika kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya SHIMIWI yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mkoani Iringa.
Akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo, Bw. Mahendeka ameanisha baadhi ya majukumu ya msingi ya watumishi wa serikali yakiwemo kutoa huduma bora kwa wananchi, kufanya kazi kwa bidiii na weledi, kuongeza tija na ubunifu pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbali mbali za utumishi wa umma.
“Watumishi wa umma tutambue kwamba sisi ndio chachu ya maendeleo ya Taifa kwani ndio tunahusika na kupanga mipango yote ya maendeleo ya nchi pamoja na utekelezaji wake. Ili kutekeleza haya yote, watumishi wa umma hatunabudi kuwa na afya njema na akili timamu na mambo haya yanapatikana kupitia kuwa na mtindo bora wa maisha na mtindo bora wa maisha ni ule unaozingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya vyakula nanvinywaji vinavyoweza kuathiri afya,” amesema Katibu Mkuu Mahendeka.
Akiwasilisha salamu toka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Taasisi iliyodhamini bonanza hilo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Bi. Khadija Mwenda, amesema udhamini huo ni sehemu ya kampeni ya OSHA ya kuhamasisha uwepo wa programu za michezo kwenye maeneo ya kazi zinazolenga kushughulikia changamoto ya kihatarishi cha kisaikolojia kinachoyakumba maeneo mengi ya kazi duniani kote.
“Ulimwengu wa kazi unakabiliwa na vihatarishi mbali mbali ikiwemo kihatarishi cha kisaikolojia (psycho-social hazard) ambacho kinapelekea matatizo mengi kwa wafanyakazi kama vile ajali na magonjwa mbali mbali yakiwemo yale yanayoathiri afya ya akili. Aidha, kumekuwa na ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile: Shinikizo la Juu la Damu, Kisukari na Saratani,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA katika salamu zake kwa watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA, kwa takwimu zilizokusanywa na OSHA katika maeneo mbali mbali ya kazi nchini katika mwaka wa fedha 2022/2023, jumla ya wafanyakazi 316,000 walipimwa afya na madaktari wa OSHA ambapo kati yao, wafanyakazi 126,400 sawa na 40% walikuwa na uzito uliozidi wastani na wafanyakazi 15,800 sawa na 5% walikuwa na Shinikizo la Juu la Damu.
“Takwimu hizi ni kiashiria kuwa wafanyakazi wengi wapo katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ambayo madhara yake hayaishii tu kwa mfanyakazi mwathirika bali hupelekea hasara kwa familia na Taifa zima kwa ujumla kwa kupoteza nguvukazi,” amesema Bi. Mwenda.
Kutokana na ukubwa wa changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza na athari zake katika uchumi wa nchi, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA ametoa rai kwa waajiri na wafanyakazi kuendelea kuzingatia ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA baada ya kufanya ukaguzi na kuchunguza afya za wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi ikiwemo kuanzisha programu za michezo mahali pa kazi.