BONANZA LA ‘SAFETY DAY’ LAFANA JIJINI ARUSHA
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeendaa bonanza la michezo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kimataifa ya usalama na afya mahali pa pazi pamoja na mwendelezo wa kampeni ya uhamasishaji wa uwepo wa mazingira salama katika maeneo ya kazi.
Bonanza hilo limekutanisha wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya kazi nchini katika michezo mbalimbali iliyofanyika katika viwanja vya shule ya kimataifa ya Breuburn jijini Arusha likihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kukimbiza kuku, kukimbia katika magunia,mbio za vijiko na ndimu pamoja na mchezo wa kuvuta Kamba n.k
Aidha katika ufunguzi wa bonanza hilo, Kamishna wa Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na wenye ulemavu) Bi. Suzan Mkangwa ambaye alikuwa mgeni rasmi amewahasa wafanyakazi kujenga utaratibu wa kushiriki michezo mbalimbali ili kuimarisha afya zao hatimaye kuzalisha kwa tija katika maeneo ya kazi.
“Tunapohimiza masuala ya usalama na afya ni lazima tuwaoneshe kwa vitendo ndio maana leo tumeandaa bonanza hili la michezo mbalimbali, tunaamini kuwa michezo inaleta undugu, inaimarisha ushirikiano pamoja na kuimarisha afya zetu ili tuweze kutekeleza kikamilifu majukumu yetu tukiwa na afya njema hivyo basi bonanza hili liwe chachu ya kila mmoja wetu kujijengea utaratibu wa kufanya mazoezi ili kujenga afya ” alisema Kamishna Mkangwa.
Aidha Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda amesema kuwa bonanza hilo ni sehemu ya uhamasishaji wa uwepo wa mazingira salama katika maeneo ya kazi kwasababu mfanyakazi anapojenga utaratibu wa kushiriki michezo anaepuka magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na mtindo mbaya wa maisha hivyo kumfanya azalishe kwa tija katika eneo lake la kazi.
Katika Bonanza hilo timu za OSHA zimeng’ara katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa pete na kuvuta kamba kwa wanaume ikishika nafsi ya pili, mchezo wa kukimiza kuku kwa wanawake na wanaume pamoja na mchezo wa kukimbia na magunia ikishika nafsi ya kwanza, mchezo wa kuvuta Kamba kwa wanaume ikishika nafasi ya pili huku timu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ikiibuka na ubingwa katika Soka na Arusha Combine wakiibuka na ubingwa katika mpira wa pete.