Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Umuhimu wa usalama na afya wasisitizwa Tanzania ikiadhimisha siku ya Usalama na Afya Duniani

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko, amewaongoza mamia ya wafanyakazi nchini kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi iliyofanyika Kitaifa Mkoani Arusha leo (Aprili 28, 2024).

Maadhimisho hayo ambayo Kauli Mbiu yake ni: Athari za mabadiliko ya tabia nchi katika usalama na afya; Sajili eneo la kazi OSHA katika harakati za kupunguza athari hizo, yamefanyika katika viwanja vya General Tyre vilivyopo Njiro Jijini Arusha ambapo yalijumuisha mamia ya wafanyakazi wa sekta mbali mbali katika Mkoa wa Arusha na mikoa mingine Tanzania Bara.

Akiwasilisha hotuba yake ya kilele cha maadhimisho hayo, Naibu Waziri Mkuu Biteko, amebainisha umuhimu wa kuhakikisha shughuli mbali mbali za kiuchumi nchini zinafanyika katika mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi.

Ameeleza kwamba jukumu la msingi Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni kuhakikisha kuwa nguvukazi ya nchi inalindwa na maeneo ya kazi yanakuwa na uzalishaji endelevu.

“Kazi yenu (OSHA) ni kufanya maeneo ya kazi yazalishe, yatengeneze ajira na wafanyakazi wafike kazini salama, watekeleze majukumu yao na kurejea nyumbani wakiwa salama na sio kutaka waajiri wawaogope au watambue nafasi yenu,” ameeleza Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Biteko.

Ameipongeza OSHA kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji ambayo yamesaidia kuboresha mahusiano baina ya OSHA na wadau wake ambapo ameitaka OSHA kuendelea kujenga utamaduni wa kuwa na mahusiano mazuri na wadau kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya uchumi wa nchi.

Aidha, ametoa wito kwa waajiri kutekeleza wajibu wao wa kuwalinda wafanyakazi hususan kwa kuwapa mahitaji yote muhimu ya kiusalama na afya ili wafanyakazi hao waweze kufanya kazi kwa furaha na kwa ufanisi mkubwa ambao utaleta tija katika uzalishaji.

Akihitimisha hotuba yake amewakumbusha waajiri na wafanyakazi kuchukua hatua ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa chanzo mojawapo cha kuzalisha vihatarishi vya ajali na magonjwa mahali pa kazi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, ambaye alimwakilisha Waziri wake, amesema Wizara ya Kazi itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na taratibu mbali mbali za Usalama na Afya kazini pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi na maelekezo yote yanayotolewa na viongozi wa juu wa Serikali.

Ameongeza kuwa jukumu hilo wanalitekeleza kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo limekuwa likisisitiza juu ya umuhimu kuzalisha kazi zenye staha.

Akitoa salamu zake baada ya kuwatambulisha wageni waliohudhuria maadhimisho hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ameeleza historia ya maadhimisho hayo ambapo amesema chimbuko lake ni wafanyakazi duniani kuandamana kwa lengo la kushinikiza waajiri wao kuwahakikishia usalama wao wanapokuwa kazini.

Aidha, Bi. Mwenda amesema malengo ya maadhimisho hayo yaliboreshwa na ILO na kujielekeza zaidi katika kufanya tafakari kuhusu hali ya usalama na afya, kutoa elimu na kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni taratibu za usalama na afya miongoni mwa waajiri na wafanyakazi.

“Nchi yetu ikiwa ni mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani, imekuwa ikiadhimisha siku hii kwa kutoa elimu kwa makundi mbali mbali ya wadau ikiwa ni pamoja na kutekeleza shughuli mbali mbali zinazolenga kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya katika sehemu za kazi ili kulinda wafanyakazi ambao ndio nyenzo muhimu katika uzalishaji,” ameeleza Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA.

Mkurugenzi Mkazi wa ILO, Bi. Caroline Khamati Mugalla, akiwa miongoni mwa wadau waliohudhuria hafla ya kilele cha maadhimisho hayo, ameipongeza Kamati ya Maandalizi kwa maandalizi mazuri yaliyofanya maadhimisho hayo kufana.

“Kauli Mbiu ya mwaka huu inaonesha kuna uhusiano mkubwa katika ya hali ya afya za wafanyakazi na mabadiliko ya tabia nchi. Athari hizo zinatukumbusha kwamba kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na kusisitiza ushirikiano baina ya serikali, waajiri na wafanyakazi katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi. Tunatoa wito kwa OSHA na wadau wa utatu kuliangalia jambo hili kwa uzito wake nasi tunawaahidi ushirikiano endelevu,” amesema Bi. Caroline Mugalla.

Kwa upande wao wadau wa utatu, Bi. Juliana Mpanduji aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Bw. Erick Swai mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kuzingatia sheria na kanuni zinazolinda afya na usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi.