Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Waziri Ndejembi afunga mafunzo ya usalama na afya, awakabidhi vifaa kinga Boda Boda wa Arusha

Na Mwandishi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi, amefunga mafunzo maalum ya usalama na afya kwa waendesha pikipiki (boda boda) wa Jiji la Arusha ambayo yametolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua vihatarishi vya ajali na magonjwa katika shughuli zao za uzalishaji.

Mafunzo hayo ni sehemu ya programu za kutoa elimu ya usalama na afya miongoni mwa makundi mbali mbali ya wajasiriamali wadogo ambayo imetolewa katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa usalama na afya mahali pa kazi.

Akihitimisha mafunzo hayo, Waziri Ndejembi amewapongeza washiriki kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo na kujitokeza kwa wingi ambapo amewataka kutumia ipasavyo maarifa waliyoyapata katika kuboresha kazi yao ya usafirishaji.

“Niwaombe ndugu washiriki pamoja na mafunzo haya, mjitahidi kuzingatia sheria za usalama barabarani na sheria nyinginezo za nchi ili muweze kutoa mchango wenu muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia kutoa huduma za usafirishaji zenye viwango stahiki,” amesema Waziri Ndejembi na kuongeza:

“Baada ya mafunzo haya sitarajii kuona mtu yoyote miongoni mwenu anakuwa sehemu ya waendesha pikipiki wanaovunja sheria za barabarani ikiwemo kuvipita vyombo vingine vya moto bila kuwa na tahadhari yoyote. Niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, inawathamini na itaendelea kuwapa mafunzo pamoja na fursa za mitaji ili muweze kujiinua kiuchumi.” 

Awali, akimkaribisha Waziri kufunga mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amewapongeza washiriki wa mafunzo kwa kujitoa na kutenga muda wao ambao wangeutumia kufanya shughuli zao za uzalishaji.

“Mheshimiwa Waziri washiriki hawa wamejitoa kweli kweli kwani tumekuwa nao hapa tangu asubuhi hadi wakati huu ambapo ni mchana hivyo tunaimani kwamba wamejifunza mambo mengi kuhusu afya na usalama kazini kwa faida yao na taifa kwa ujumla,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Boda Boda Wilaya ya Arusha, Bw. Okelo Costantine, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwapigania vijana kufanya kazi zao kwa utulivu pamoja na kuwapatia fursa mbali mbali zikiwemo za mafunzo.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika leo (Aprili 29, 2024) katika Uwanja wa General Tyre uliopo Njiro Jijini Arusha, yalijumuisha mada mbali mbali zikiwemo utambuzi wa vihatarishi vya usalama na afya katika shughuli za usafirishaji pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza kwa waathirika wa matukio ya ajali za barabarani. Aidha, washiriki hao walikabidhiwa baadhi ya vifaa kinga yakiwemo mavazi yanayomtambulisha mtu akiwa katika eneo la kazi (reflective vests) ambayo yamegharamiwa na serikali kupitia Taasisi ya OSHA.