Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

KATIBU MKUU KAZI AWATAKA WATENDAJI OSHA KUJITUMA KATIKA UTENDAJI

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Maganga, amewataka watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kutekeleza majukumu yao kwa bidii pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma zao katika kufanikisha malengo ya Taasisi hiyo yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi nchini.

Ametoa wito huo jana (28/05/2024) alipofanya ziara katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam kwa lengo kujionea namna OSHA inavyotekeleza majukumu yake ikiwa ni miongoni mwa Taasisi chini ya Wizara anayodumu tangu alipohamishiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira mnamo Machi 31, 2024.

Bi. Mary aliwasili katia Ofisi za OSHA majira ya Saa 3:00 Asubuhi na kufanya kikao kifupi na Menejementi ya OSHA ambapo alipokea taarifa kuhusu OSHA na majukumu inayotekeleza kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda. 

Katika wasilisho lake, Bi. Mwenda aliielezea Taasisi ya OSHA akigusia masuala kama vile muundo wa Taasisi, Historia, Dira, Dhima na Tunu, majukumu ya Taasisi, utekelezaji wa Mpango Mkakati wasasa ikiwemo mafanikio na changamoto za kipindi cha hivi karibuni.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya Mtendaji Mkuu, Katibu Mkuu Bi. Maganga, aliipongeza OSHA kwa hatua kubwa iliyopiga katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi hususan kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

“Kazi yenu naiona kama wito kwani haifanyiki kwa ajili ya kupata kipato bali kwa ajili ya kusaidia watu watekeleze majukumu yao wakiwa katika mazingira salama kwahiyo mkitekeleza wajibu wenu ipasavyo basi tutaleta mabadiliko makubwa sana katika maendeleo ya Taifa letu kwakuwa tija katika uzalishaji itaongezeka,” ameeleza Bi. Maganga na kuongeza: 

“Mimi nawaamini sana na kwa taarifa na nyaraka nilizozipitia hapa naona kuna weledi wa kutosha ndani ya Taasisi hii kwahiyo ni juu yetu kubaki kuwa vinara. Tujitahidi ili tuweze kuacha alama na hata tukistaafu tuwe na uwezo wa kutembea kifua mbele na kueleza mambo ambayo tulichangia kuyafanikisha tukiwa ndani ya Taasisi hii.”

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Usimamizi huu hufanyika kupitia usajili wa maeneo ya kazi na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba inakidhi viwango stahiki.