Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

Frequent Asked Questions

  • 1 OSHA ni nini?
    Ni kifupi cha maneno ya kiingereza- ‘Occupational Safety and Health Authority’-OSHA ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
  • 2 Taasisi inayojihusika na masuala gani?
    Ina jukumu la kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi yanakuwa salama dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuwasababishia wafanyakazi ajali ama magonjwa kutokana na kazi wanazozifanya. 
  • 3 OSHA ipo tangu lini?
    Ilianzishwa rasmi mwaka 2001 na Sheria yake kupitishwa na Bunge mwaka 2003 ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Serikali wa maboresho katika utoaji huduma kwa umma yaliyofanyika kupitia Sheria Na. 30 ya Wakala za Serikali ya mwaka 1997 (Executive Agencies Act).
  • 4 Majukumu yanayotekelezwa na OSHA ni yapi?
    Taasisi hii ina majukumu makuu manne ambayo ni;

    Kusimamia Utekelezaji wa Sheria Namba 5 ya mwaka 2003 ya Usalama na Afya na Mahali pa Kazi.
    Kushauri serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, kuhusiana na sera, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa Usalama na Afya Nchini ikiwemo kushauri namna ya kuridhia mikataba ya kimataifa kuhusu masuala ya Usalama na Afya.
    Kuongeza uelewa miongioni mwa wadau kususiana na masuala ya Usalama na Afya kwa kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau
    Kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usalama na afya katika sehemu za kazi ili kuweza kushauri serikali namna bora ya kutekeleza sheria tajwa.
  • 5 Shughuli za kila siku za OSHA ni zipi?
    Wakala hufanya shughuli mbali mbali zikiwemo;

    Kusajili sehemu za kazi.
    Kufanya ukaguzi wa jumla (General Inspections) na ukaguzi maalum (specific inspections) mfano ukaguzi wa usalama wa umeme, vyombo vya kanieneo (Pressure vessels) na ukaguzi wa vifaa vya kunyanyulia vitu vizito (Lifting appliances).
    Kutathmini hatari zilizopo mahali pa kazi (Risk assessment).
    Kufanya mapitio ya michoro na majenzi ya sehemu za kazi.
    Kufanya uchunguzi wa Afya na magonjwa kulingana na kazi husika mahali pa kazi.
    Kufanya uchunguzi wa ajali (accident investigation).
    Kufanya tathmini ya athari za kimazingira (Industrial hygiene surveys and measurements). Kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu masuala ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi.
  • 6 Nawezaje kupata huduma za OSHA?
    Huduma za OSHA zinapatikana nchi nzima kupitia Ofisi zetu zilizopo kwenye Kanda sita (6) pamoja na baadhi ya mikoa Tanzania Bara au kupitia njia mbali mbali za mawasiliano. Hivyo, ukihitaji huduma zetu tafadhali wasiliana na Mtendaji Mkuu kupitia S.L.P 519 Dar es Salaam, Barua Pepe: info@osha.go.tz. Tembelea tovuti yetu: www.osha.go.tz au tupigie kwa namba ya Bure 0800110091/0800110092 nasi tutakuhudumia.
  • 7 OSHA hufanya kaguzi za aina gani?
    Kaguzi zinazofanywa na OSHA katika sehemu za kazi ni kwa mujibu wa Sheria Namba 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, Sura Namba 297. Kaguzi hizo ni pamoja na; Ukaguzi wa Jumla, Ukaguzi wa Usalama wa Mitambo, Ukaguzi wa Usalama wa Umeme, Ukaguzi wa Viwango vya Mazingira ya kazi, Ukaguzi wa Egonomia na Ukaguzi wa Usalama katika shughuli za Ujenzi. Kaguzi hizi hufanyika kulingana na mpango kazi ambao ni kuhakikisha sehemu ya kazi inakaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na kufuatiwa na kaguzi za ufuatiliaji. Aidha ukaguzi unaweza kufanyika muda wowote endapo kuna haja ya kufanya hivyo.
  • 8 OSHA hufanya kaguzi za aina gani?
    Kaguzi zinazofanywa na OSHA katika sehemu za kazi ni kwa mujibu wa Sheria Namba 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, Sura Namba 297. Kaguzi hizo ni pamoja na; Ukaguzi wa Jumla, Ukaguzi wa Usalama wa Mitambo, Ukaguzi wa Usalama wa Umeme, Ukaguzi wa Viwango vya Mazingira ya kazi, Ukaguzi wa Egonomia na Ukaguzi wa Usalama katika shughuli za Ujenzi. Kaguzi hizi hufanyika kulingana na mpango kazi ambao ni kuhakikisha sehemu ya kazi inakaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na kufuatiwa na kaguzi za ufuatiliaji. Aidha ukaguzi unaweza kufanyika muda wowote endapo kuna haja ya kufanya hivyo.

  • 9 Je ni mafunzo gani ambayo hutolewa na OSHA?
    OSHA hutoa mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuboresha Mazingira ya kazi, mafunzo hayo ni pamoja na Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi (National Occupational Safety and Health Course-NOSHC), Tathimini ya vihatarishi vya Usalama na Afya (OHS Risk Assessment), Kufanya kazi kwenye maeneo ya juu (Working at Height), Kozi ya Wawakilishi wa Kamati za Usalama na Afya (Safety and Health Representatives Course), Usalama katika matumizi ya Kemikali mahali pa kazi (Safe use of chemicals), Usalama na Afya katika Ujenzi (Safety and Health in construction industry), Mafunzo ya Uchunguzi wa Ajali (Accident Investigation), Mafunzo ya Huduma ya Kwanza (Industrial First Aid) pamoja na Uelewa  wa jumla wa masuala ya usalama na Afya (General OHS Awareness).
  • 10 Je kama na eneo dogo la wafanyakazi wa tatu naweza kujisajili OSHA?
    Sheria inasema kila eneo la kazi linatakiwa kusajiliwa na OSHA ili liweze kuingizwa kwenye daftari la Mkaguzi Mkuu wa sehemu za kazi nchini na kufikishiwa huduma za ukaguzi.
  • 11 Nini faida ya kusajiliwa na OSHA?
    Kwanza ni kukidhi matakwa ya Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na kutambuliwa na OSHA ili kuweza kupatiwa huduma za kaguzi, hii itakusaidia kupata miongozo ya kuwakinga wafanyakazi wako wasiumie au kupata magonjwa wakiwa kazini ikiwemo kupata ushauri wa kitaalam kuhusu masuala ya Afya na Usalama mahali pa kazi. Hii pia itakusaidia mwajiri kuwa na wafanyakazi wenye Afya njema na watakaofanya kazi kwa kujiamini na hivyo kuongeza tija katika eneo lako la kazi.
  • 12 Kuna tofauti yeyote ya upimaji wa Afya unaofanywa na OSHA pamoja na ule unaofanywa na Manispaa?
    Upimaji wa Afya kwa wafanyakazi unaofanywa na madaktari katika hospitali za kawaida na ule unaofanywa na madaktari wa OSHA ni tofauti. Katika hospitali za kawaida mara nyingi upimaji huo unafanywa kwa lengo la kubaini uwepo au uwezekano wa kusababisha magonjwa ya mlipuko ili yasiwadhuru wateja mfano: Kipindupindu, Taifodi nk. Wakati madktari wa OSHA wanaangalia magonjwa yatokanayo na kazi na hufanyika katika hatua tatu yaani anopa ajiriwa kwa mara ya kwanza, akiwa kazini na anapotoka kazini (akiwa ameacha kazi, amefukuzwa au akiwa anastaafu) kwa mujibu wa Sheria.
  • 13 Kuna Viwango (standard) zozote za PPE na zipoje?
    Viwango vipo kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ndilo lenye jukumu la kuweka na kusimamia viwango mbalimbali vya ubora wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na zinazotengenezwa nchini. Aidha kanuni ya matumizi sahihi ya vifaa kinga kazini, utunzaji wake pamoja na ubora kulingana na kazi zinazofanywa huandaliwa na kusimamiwa na OSHA.
  • 14 Kwenye shughuli za ujenzi kazi nyingi ndogo ndogo hufanywa na vibarua ambao hawana mikataba je wanatakiwa kupimwa afya?
    Sheria ya Mahusiano kazini haitambui ajira ya vibarua bali wafanyakazi wa mkataba hivyo kundi hilo la watu wanaofahamika kama vibarua wana haki sawa kabisa na wafanyakazi wengine, kupatiwa huduma za OSHA kama kupima Afya zao, kupewa vifaa vya kujikinga na huduma nyinginezo

  • 15 OSHA inatambua ugonjwa wa Ukimwi katika sehemu za kazi?
    OSHA inatambua ugonjwa huo kama ambavyo shirika la Afya Duniani linavyoelekeza, kila eneo la kazi pawepo sera ya Ukimwi na kuna muongozo wa jinsi ya kuandaa sera hizo kwa mujibu wa TACAIDS, hivyo tunapotembelea maeneo ya kazi kwa ajili ya kufanya ukaguzi huwa tunaangalia pia uwepo wa sera ya Ukimwi.
  • 16 Je ni kila mwaka natakiwa kuwa na cheti cha kukidhi matakwa?
    Ni kweli kila mwaka mwajiri anatakiwa kupata cheti cha kukidhi matakwa ya awali ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Compliance Lincense) baada ya kufanyiwa kaguzi, kupima Afya wafanyakazi na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wake yaani (Huduma ya Kwanza na mafunzo kwa wana kamati za Usalama na Afya)
  • 17 Fidia kwa mtu anayeumia kazini ikoje?
    OSHA haitoi fidia kwa Mfanyakazi yeyote anayeumia akiwa kazini kwani sheria inayosimamiwa na OSHA inalenga kumkinga mfanyakazi asiumie au kupata magonjwa akiwa kazini, endapo utaumia ukiwa kazini, utalazimika kufuata taratibu za kuomba huduma ya matibabu au fidia kutoka katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
  • 18 Nawezaje kujiunga mafunzo ya Afya na Usalama mahali pa kazi yanayotolewa na OSHA?
    Kujiunga na mafunzo ya OSHA tembelea Ofisi za OSHA zilizopo karibu nawe au  tembelea tovuti ya OSHA www.osha.go.tz utaweza kupata taarifa juu ya mafunzo yatolewayo  na OSHA namna ya kujiunga.
  • 19 Je OSHA inakagua gereji?
    Ndio, gereji ni eneo la kazi kama maeneo mengine, hivyo hukaguliwa ili kushauri kuhusu taratibu na uwekaji wa mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vitokanavyo na shughuli hizo.
  • 20 Je OSHA inawakagua wenye Boda boda ?
    OSHA haifanyi ukaguzi kwa waendesha piki piki (boda boda) ambao hukaguliwa kulingana na Sheria ya Usalama barabarani japokuwa kama watakuwa na maeneo rasmi wanayofanyia kazi kama ofisi na karakana za matengenezo, zinaweza kusajiliwa na kukaguliwa kama maeneo mengine ya kazi.